Ticker News

Your Ad Spot

Thursday, July 25, 2024

IJUE SHULE YA SEKONDARI KALIUA, NI YA TAHASUSI (MICHEPUO) YA SAYANSI

Kaliua, Tabora
Shule ya Sekondari ya Kaliua iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ambayo sasa ina hadi Kidato cha sita, ni miongoni mwa shule za sekondari nchini ambazo zinafanya vizuri katika ufaulu wa wanafunzi ikiwa ni ya tahasusi au michepuo ya Sayansi tu.

Kufuatia jitihada za walimu wakishirikiana na Bodi ya shule na serikali hususan Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua shule iliazimia kufuta daraja sifuri (0) na nne (IV), mwaka 2017 na azimio hilo likaanza kuzaa matunda kuanzia mwaka 2018.

Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Mussa Ngonile Mwasile, anasema, kwa mfano kufuatia mkakati huo, ufaulu wa Kidaco cha Sita mwaka 2022 Watoto 139 walipata divisheni 1, 88 wakipata divisheni II na watano (5) tu ndiyo waliopata divisheni III, huku kukiwa hakuna aliyepata divisheni IV au 0.

Anasema, Katika matokeo mwaka huu wa 2024, Watoto 154 wametwaa daraja la kwanza (Div I), 78 wakatwaa divisheni II na wawili hiyo ndiyo waliopata divisheni III, huku kukiwa pia hakuna aliyepata divisheni IV wala daraja 0.

Bila shaka matokeo hayo ni ishara halisi kwamba shule ambayo ina mchanganyiko wa wanafunzi wa kike na wa kiume, inaunga mkono kwa vitendo mkakati wa Serikali ya ya Tanzania, hususan ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk, Samia Suluhu Hassan, wa kutia mkazo wanafunzi hasa wa kike kusoma na kufaulu kwa wingi masomo ya sayansi.

Kwa ufaulu unaoonekana Shule ya sekondari ya Kaliua ni dhahiri itachangia kwa kiwango kinachokusudiwa na nchi cha kupata wataalam kama madaktari, wahandisi, walimu wa sayansi, manesi, wataalamu wa maabara na kilimo, kwa kuwa ni shule yanye tahasusi za sayansi tu kama PCM, PCB, PGM, PMC na PCB.

Shule ya Sekondari ya Kaliua, ilianza rasmi mwaka 1997 kwa kwa namba ya usajili S0697, na ilianza na kidato cha kwanza tu, ikiwa na wanafunzi 85.

Kwa mujibu wa
Mwalimu Ngonile, kuanzishwa shule hiyo kulitokana mwamko wa elimu wa Wananchi hususa wazazi waliokuwa wakiishi Kaliua wakati huo ikiwa Kata na hakuna shule, hivyo wakaazimia kuanzisha shule kunusuru watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda kusoma shule za mbali.

Mwalimu Ngonile, anasema, kutokana na changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu na hivyo kuwa katika mazingira hatarishi, Wazazi au Wananchi wa Kata hiyo kwa jumla wakaamua kuchangia nguvu kazi na fedha kupitia makato ya kodi ya zao la tumbaku ambalo ni miongoni mwa mazao makubwa ya biashara mkoani Tabora.

Kufuatia juhudi na mshikamano wa Wananchi mwaka huo wa 1997 shule ya Sekondari ya Kaliua ikaanzishwa rasmi Mkuu wa kwanza akiwa Simon Kyala. Ilianzishwa ikiwa na wanafunzi 85 tu, na baada ya hapo shule ikawa kimbilio la wananchi na sasa ina jumla ya Wanafunzi 2053 wakike na wakiume.

Kila penye mafanikio ni nadra kukosekana changamoto, hivyo licha ya shule hiyo kuwa na mafanikio lukiki ikiwemo ufaulu wa juu, inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kuwa na idadi walimu wasiotosha wa sayansi ambao ni 17 wakati wanaohitajika kulingana na uwiano wa wanafunzi 2053 waliopo ni walimu 22.

Kwa mujibu wa 
Mwalimu Ngonile kwa sasa changamoto hiyo imepunguzwa na Wazazi walioamua katika vikao vyao na uongozi wa shule kusaidia kuajili walimu kadhaa.


Anataja changamoto nyingine, ni shule kukosa gari kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kuwapeleka wanafunzi kwenye matibabu wanapougua kiasi cha kutoweza kubebwa kwenye pikipiki, hivyo taratibu mbalimbali zinafanyika kwa kushirikiana uongozi wa shule na serikali kuondoa changamoto hiyo.

Anasema, kutokana na changamoto hiyo mwanafunzi akiungua kiasi cha kutoweza kubebwa kwa pikipiki hutumika gari la Mkuu wa shule kumuwahisha kwenye matibabu.

Akizungumzia mkakati wa shule kwenda kwenye mafanikio zaidi 
Mwalimu Ngonile anasema, shule imejipanga kuhakikisha kila mwanafunzi anayemaliza kidato cha sita anapata daraja la kwanza (div I) la poiniti 3-5 tu, na kwa kidato cha nne ni kuondoa daraja la nne na tatu.

Kuhusu siri ya mafanikio iliyonayo shule hiyo,
Mwalimu Ngonile anafichua kuwa yametokana na juhudi za Walimu, Bodi ya shule na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kaliua kufanya kila mbinu kuhakikisha shule inakuwa bora hasa kwenye kupata ufaulu wa juu kwa wanaohitimu kidato cha nne na cha sita.

Miongoni mwa juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa hasa na uongozi kuhakikisha shule inapiga hatua kubwa ni kuwawezesha walimu kwa njia mbalimbali za kuwatia ari ikiwemo kuwapa motisha wanapofanikisha matokeo mazuri ya ufaulu.

Mwalimu Ngonile anasema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kaliua Jerry Mwaga, amekuwa akitoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri huku Bodi ya shule nayo ikitoa motisha kwa waliofanya vizuri na hata waliofanya vibaya, jambo ambalo limewajengea walimu ari ya kuchapa kazi kwa bidii hivyo kuleta matokeo chanya.

Chachu nyingine ni utayari wa walimu kuleta matokeo chanya kwa ushawishi na umoja waliojiwekea kwa kushirikiana na mkuu wa shule ambao umewezesha kila mmoja kujituma katika ufundishaji na kusimamia kwa dhati nidhamu.


Mwalimu Ngonile anasema, usimamizi wa nidhamu umewezesha wanafunzi kukubali mabadiliko na kuwa na nidhamu ya kusoma kwa bidii na ya kusimama imara katika ndoto zao wawapo ndani na nje ya shule, jambo ambalo limeweza kuibua ufaulu mzuri.

Anahitimisha kwa kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita Dk. Samia Suluhu Hassan na Wasaidizi wake wote, kwa kutoa kipaumbele katika kuhakikisha shule zinakuwa bora kitaaluma kwa kuziwekea miundombinu bora ya kufundishia na kujifunza kama madarasa, nyumba za walimu, maabara na vitabu.

Mwalimu Ngonile pia amempongeza Rais Dk. Samia kwa uamuzi wa kutoa fursa ya elimu bila ada hadi kwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita.


Mpango huo wa wanafunzi wa kidato cha tano na sita kusoma bila ada ulipitishwa rasmi Bungeni katika Bajeti ya Serikali Kuu ya 2020/2023.

Kabla ya hapo mpango wa elimu bila ada ulianza mwaka 2015 katika Serikali ya Awamu ya tano ukihusu kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwalimu Ngonile akaweka wazi kwamba kufuatia kufuta ada kwa wanafunzi hadi kidato cha sita kumeleta ahuweni kubwa kwa shule kuachana na mambo ya kukimbizana na wazazi kuhusu suala la ada na pia limetoa nafuu kubwa kwa wazazi hasa wenye kipato kidodo ambao walikuwa hawawezi kumudu ada za watoto.

Anasifu kwamba jambo hilo limeleta afya zaidi kwenye sekta ya elimu kwa sababu sasa kila mzazi au mlezi anamudu kupeleka watoto shule tofauti na awali.

 
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kaliua

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages